Exodus 30

Madhabahu Ya Kufukizia Uvumba

(Kutoka 37:25-28)

1 a“Tengeneza madhabahu kwa mbao za mshita kwa ajili ya kufukizia uvumba. 2 bMadhabahu hayo yawe mraba, urefu na upana wake dhiraa moja,
Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45.
na kimo cha dhiraa mbili,
Dhiraa mbili ni sawa na sentimita 90.
nazo pembe zake zitakuwa kitu kimoja nayo.
3 eFunika hayo madhabahu juu na pande zote na pia pembe zake kwa dhahabu safi, na uifanyizie ukingo wa dhahabu kuizunguka. 4 fTengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, ziwe mbili kila upande, za kushikilia hiyo mipiko itumikayo kuibebea madhabahu. 5 gTengeneza mipiko kwa miti ya mshita na uifunike kwa dhahabu. 6 hWeka hayo madhabahu mbele ya lile pazia lililo mbele ya Sanduku la Ushuhuda, lililo mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya Sanduku la Ushuhuda, mahali ambapo nitakutana nawe.

7 i“Itampasa Haruni kufukiza uvumba wenye harufu nzuri juu ya madhabahu kila siku asubuhi wakati anapowasha zile taa. 8 jItampasa afukize uvumba tena wakati anapowasha taa wakati wa machweo ili uvumba ufukizwe daima mbele za Bwana kwa vizazi vijavyo. 9 kUsifukize uvumba mwingine wowote juu ya madhabahu haya au sadaka nyingine yoyote ya kuteketezwa wala sadaka ya nafaka, wala usimimine sadaka ya kinywaji juu yake. 10 lMara moja kwa mwaka Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe za hayo madhabahu. Upatanisho huu wa mwaka lazima ufanywe kwa damu ya sadaka ya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa vizazi vijavyo. Ni takatifu sana kwa Bwana.”

Fedha Ya Upatanisho

11Naye Bwana akamwambia Musa, 12 m“Utakapowahesabu Waisraeli, kila mmoja lazima alipe kwa Bwana fidia kwa ajili ya nafsi yake wakati wa kuhesabiwa kwake. Ndipo hakutakuwa na pigo juu yao unapowahesabu. 13 nKila mmoja anayekwenda upande wa wale waliokwisha hesabiwa atatoa nusu shekeli,
Nusu shekeli ni sawa na gramu 6.
kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini.
Gera 20 ni sawa na shekeli moja au gramu 12.
Hii nusu shekeli ni sadaka kwa Bwana.
14 qWote wale wanaovuka, wenye umri wa miaka ishirini au zaidi, watatoa sadaka kwa Bwana. 15 rMatajiri hawatalipa zaidi ya nusu shekeli, nao maskini hawatatoa pungufu wakati mnatoa sadaka kwa Bwana kwa kufanya upatanisho wa nafsi zenu. 16 sUtapokea fedha ya upatanisho kutoka kwa Waisraeli na uzitumie kwa ajili ya huduma ya Hema la Kukutania. Itakuwa ni ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Bwana kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu.”

Sinia La Kunawia

17Kisha Bwana akamwambia Musa, 18 t“Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake. 19 uHaruni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji yatokayo katika hilo sinia. 20 vWakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili kwamba wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, 21 wwatanawa mikono na miguu yao ili kwamba wasije wakafa. Hii itakuwa ni amri ya kudumu kwa ajili ya Haruni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.”

Mafuta Ya Upako

22 xKisha Bwana akamwambia Musa, 23 y“Chukua vikolezi bora vifuatavyo: shekeli 500
Shekeli 500 ni sawa na kilo 6.
za manemane ya maji, shekeli 250
Shekeli 250 ni sawa na kilo 3.
za mdalasini wenye harufu nzuri, shekeli 250 za miwa yenye harufu nzuri,
24 abshekeli 500 za aina nyingine ya mdalasini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, pia hini
Hini moja ni sawa na lita 4.
ya mafuta ya zeituni.
25 adVitengeneze vikolezi hivi kuwa mafuta matakatifu ya upako yenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Yatakuwa mafuta matakatifu ya upako. 26 aeKisha yatumie kupaka hilo Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda, 27meza na vifaa vyake vyote, kinara cha taa na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, 28madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote na sinia pamoja na kitako chake. 29 afUtaviweka wakfu ili viwe vitakatifu sana na kila kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.

30 ag“Mtie Haruni na wanawe mafuta na uwaweke wakfu ili waweze kunitumikia katika kazi ya ukuhani. 31 ahWaambie Waisraeli, ‘Haya yatakuwa mafuta matakatifu yangu ya upako kwa vizazi vijavyo. 32Usiyamimine juu ya miili ya wanadamu wala usitengeneze mafuta ya aina nyingine kwa utaratibu huu. Ni mafuta matakatifu na ni lazima myaone kuwa ni matakatifu. 33 aiMtu yeyote atakayetengeneza manukato kama hayo na yeyote atakayeyamimina juu ya mtu yeyote ambaye si kuhani atakatiliwa mbali na watu wake.’ ”

Uvumba

34 ajKisha Bwana akamwambia Musa, “Chukua vikolezi vyenye harufu nzuri vifuatavyo: natafi, shekelethi, kelbena na uvumba safi vyote vikiwa na vipimo sawa, 35 akpia tengeneza mchanganyiko wa uvumba wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Utiwe chumvi ili upate kuwa safi na mtakatifu. 36 alSaga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali ambapo nitakutana nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu. 37Msitengeneze uvumba mwingine wowote wa namna hii kwa ajili yenu wenyewe; uoneni kuwa ni mtakatifu kwa Bwana. 38Yeyote atakayetengeneza uvumba kama huu ili kufurahia harufu yake nzuri lazima akatiliwe mbali na watu wake.”
Copyright information for SwhKC